Thursday, May 20, 2010

MAKALA:BILA KUWATHAMINI WACHEZAJI WETU HATUTAFIKA POPOTE

Asalaam aleikhum wasomaji wote wa jarida hili la number 10,jarida lililoweza kumaliza kiu ya wapenda soka kwa kuwapa taarifa muhimu  na kutoa mustakabali wa soka letu jinsi linavyoenda na nini kifanyike ili tuweze kukuza soka letu ba hatimae kufikia malengo ya juu na kiwango cha kimataifa.

Leo ningependa kuongelea jinsi timu zetu zinavyomaliza vipaji vya wanasoka wetu na bila hata kuonyesha kuwa wanathamini michango yao katika maendeleo ya soka katika timu husika na hata katika maendeleo ya timu yetu ya taifa.
Tanzania ni nchi yenye wanasoka wenye  vipaji vya hali ya juu  sana tatizo ni viongozi wa timu zetu hawana upeo wa kuona hili tena na kwasababu wengi wao hugombea nafasi za uongozi kwenye klabu hizi kubwa za Simba na Yanga kwa nia zao binafsi za kupata umaarufu na kujulikana ili baadae waweze kugombea ubunge au kupata nafasi za kupata biashara na kuongeza mitandao yao ya kibiashara na sio kuiendeleza timu husika.
Ni jambo lililo wazi kuwa klabu hizi za Yanga na Simba ni timu zilizoanzishwa zaidi ya miaka 30 iliyopita lakini  cha kushangaza ni timu ambazo hazina uwezo wa kujiendesha wala kuweza kulipa mishahara ya wachezaji wake mpaka karne hii ya sasa,Yanga na Simba zilipaswa kuwa kama timu za kisasa  kama Asante Kotoko,Asec Mimosas,Orlando Pirates,Kaizer chief  na nyingine nyingi zenye uwezo wa kifedha na rasilimali nyingi.lakini cha kushangaza  mpaka leo wachezaji wa Simba na Yanga pamoja na mbwembwe zote za viongozi mpaka sasa hutegemea mishahara toka kwa wafadhili binafsi na kufanya wachezaji kuishi maisha ya ajabu na kukosa morali ya kucheza soka makini.

                   Pichani kulia ni Pawasa na kushoto ni Ally Mayay mchezaji wa zamani wa yanga 

Tatizo kubwa la  viongozi wa klabu hizi wana mitazamo ya kizamani ya kuamini kuwa kuifunga timu pinzani ndio mafanikio ya kipindi cha uongozi wake klabuni na wala sio kuiwezesha timu kufikia kuchukua vikombe kwenye michuano mikubwa afrika,hii ni mitizamo ya ajabu sana kwa viongozi hawa wetu wa klabu hizi kubwa za Simba na Yanga.ndio maana hata kocha mpya wa Yanga Afrika ameshangaa kuona viongozi wake wanaiweka timu kambini Hoteli ya Holiday eti kwa maandalizi ya mechi ya samba na wakati wa maandalizi ya mechi ya Fc Lumpopo timu iliwekwa kambini pale klabuni jangwani.hivi hata kwa mwenye fikra ndogo atashangaa,hivi mafanikio kwa viongozi wa Yanga ni kuifunga Simba tu na wala sio kusonga mbele kwenye michuoano ya klabu bingwa afrika na kuiwezesha klabu kupata mapato makubwa na kuweza kujijengea jina kubwa Africa?Haya ndio mambo yanayowavunja nguvu wachezaji na kuweweka katika kipindi kigumu kuwaza mechi ya samba vs yanga na kuacha kuwaza jinsi ya kujiendeleza kisoka.
Aaron Mwinula  Nyanda aka Nua na Boniface Pawasa aka Jancker  ni mifano ya wachezaji walioweza kuzisaidia timu zao za  Simba na Yanga kuweza kuchukua mataji mengi ya ligi na michuano mingine mingi wakiwa na timu hizi,lakini waliamua kukimbilia chuoni Cbe  kusoma ni baada ya kuona soka letu limejaa mizengwe na viongozi wa timu hizi kutowathamini,hivi si ni aibu kubwa kwa timu kama Yanga au Simba kumuacha mchezaji kwenye usajili eti kisa ameumia mguu.mifano halisi ya wachezaji kama Marehemu Kipa  Riffat Said alivunjika mkono kwenye ajali akiwa na timu yake ya  Yanga na akakatwa kwenye usajili bila hata kumfidia, hivi viongozi wetu huwa hawajui hii inaua soka letu???hivi mchezaji anapoiwezesha klabu kushinda mechi zote za ligi halafu anazungushwa msahahara wake na posho zake  na viongozi hii nayo ni nini?ni lini viongozi wetu hawa wataamua kuelezwa ukweli na wachezaji wao na kuchukua maoni toka kwa wachezaji wao ili kutengeneza mikakati ya kuiwezesha klabu zao  kuwa imara na kuweza  kujitegemea.
Kwangu mimi kama ningekuwa mpiga kura wa kuchagua kiongozi wa klabu hizi ningefata sifa hizi, kiongozi bora  wa soka awe na mitazamo hii mitatu,kwanza ajue klabu imetoka wapi,pili ajue klabu ipo wapi sasa,na tatu klabu inatakiwa kwenda wapi kimaedeleo.

 La kwanza ni muhimu sana kwa kiongozi anayeomba uongozi kwenye timu hizi awe anajua klabu imetokea wapi na ina matatizo gani inayokumbana nayo ili kuweza kutengeneza mipango ya kuweza kufanya mapinduzi kwenye soka na sio kuongoza kwa mazoea kwamba lengo na mipango yake ya uongozi ni kuifunga timu pinzani tu kwenye ligi ya ndani,hili ndio linafanya mpaka sasa timu hizi kubwa za Simba na Yanga kukosa kuwa na wadahamini madhubuti kama timu nyingine za afrika.hakuna kampuni yeyote dunani itakayoamua kuidhamini timu ambayo haina mipango madhubuti na uongozi imara,maana tujue wazi kwenye mambo ya udhamini ni makubaliano ya  nipe nikupe kwa maana ya kwamba timu inapata fedha na vifaa na kampuni iweze kujitangaza kupitia timu hiyo sasa pale timu inapokosa kupata mafanikio inaharibu mpaka jina la bidhaa inayotangaza,ni aibu sana kwa Hizi timu zetu za simba na yanga karne hii bado wanategemea mapato ya milangoni na misaada toka kwa wafadhili binafsi na sio makampuni ambayo yangedhidhamini klabu hizi.Hii ni  aibu kubwa kwa timu hizi kubwa kuacha watu wachache kujipatia utajiri kwa kuuza bidhaa zenye nembo ya klabu hizi na bila hata ya  klabu hizi kupata gawiwo lolote.wakati timu zote duniani huingiza pesa nyingi kwa kuuza bidhaa za klabu kama jezi,bandama,bendera hata stika za klabu hizi,dunia nzima hii ni biashara ambayo hata Real Madrid huuingiza pesa nyingi kwa wapenzi kununua jezi za klabu zao,Yaani Simba na Yanga hawana hata duka moja la kuuza bidhaa zao kama jezi na bendera na kuwaachia watu wacheche kujinufaisha kwa kutumia nembo hizi za klabu kwa manufaa yao.
Je viongozi wa simba na yanga hawalioni hili?au ndio yale niliyoyasema mwanzo ya kuongoza hizi timu  kwa mazoea???



Kwa la pili la kujua klabu ipo wapi sasa kwa hili kiongozi huyu anapaswa kutatua matatizo yanayoikabili klabu kama kupata wadhamini watakaoiwezesha klabu kuwa na uwezo wa kuwalipa wachezaji wake na kuwafanya waishi maisha yanayolingana na timu hizi kubwa za simba na Yanga,hii ni kuwawezesha wachezaji wake kupata bima za afya na familia zao,malazi salama haya yatawafanya wachezaji wetu kucheza kwa bidii na kuamini wapo kwenye njia sahihi maana kwa soka letu la sasa mchezaji wa soka akipata uhakika wa kupata chuo cha kusoma ni rahisi sana kwake kuacha soka ili akasome na hatimae kupata kazi itakayomsaidia katika maisha yake ya mbele,kwa hili tutajenga kizazi ambacho kitakosa wachezaji wenye vipaji na wasomi katika timu zetu.

La tatu ni kujua klabu inatakiwa kwenda wapi.katika hili kiongozi anapaswa kuwa na mipango makini ili kuweza kuifikisha timu katika mafanikio makubwa,mafanikio kwangu mimi ni kuiwezesha timu kupata vikombe vingi vya ndani na kimataifa na kuifanya timu iweze kujiendesha kibiashara kwa kuuza wachezaji na kuanzisha miradi ya kuendeleza soka la watoto ili baadae waweze kuchezea timu ya wakubwa.kwa hili viongozi hawa wa timu zetu wataweza kuisaidia TFF na kocha wa timu ya taifa kuwa na wachezaji bora na watakaoiwezesha nchi hii kupata mafanikio na kukuza soka pia.
Hili la viongozi wa klabu zetu kubwa kukosa mipango juu la soka la watoto ndio linaleta matatizo ya viongozi wa klabu zetu kuwang’ang’ania wachezaji pale wanapopata timu nje ya nchi.hii inasababishwa hasa na timu kutokuwa na mipango ya muda mrefu  na kukosa dira kwa viongozi wanaona kuwa mchezaji wao akiondoka watakosa mwingine wakuwasaidia,hili ni jambo linalowaumiza sana wachezaji wetu wengi inapofikia wakati viongozi wa klabu wanapokataa kutoa ruhusa na vibali(ITC) kwa wachezaji wao wanapopata timu nje ya mipakea yetu. Kwa mtazamo wangu nilidhani viongozi hawa wangefurahia hili na kukubali kuuza wachezaji nje ili watumie hizo hela za kuuza wachezaji kusajili wachezaji wengine na kuboresha timu za watoto wadogo  ili waweze kukuza vipaji vyao na  na kuiwezesha klabu kufikia malengo sahihi.ni aibu kubwa kwa viongozi hawa kuwangangania wachezaji hawa waliosajili kwenye timu zao  wasijiunge na timu nyingine nje ya nchi yetu na waweze kuendeleza soka lao na kuitangaza nchi kimataifa na kuisadia timu yetu ta taifa kwenye michuano ya kimataifa,hivi bila hawa wakubwa kusogea na kupata timu nje wale wachezaji wadogo wa Simba B na Yanga B wataenda kucheza wapi sasa???hebu ona mifano ya nchi kama Ghana na Senegal walivyopeleka vijana wao ufarasa na ubelgiji na kwingine nchi za scandanavia na baadae kupata mafanikio makubwa kwenye soka lao.

Kwani Jerry Tegete au Mrisho Ngassa kwa Yanga ni alfa na omega???ni aibu kuona eti mchezaji  anakatishwa  majaribio ili aweze kusaini mkataba wa timu nje ya nchi ili kuja kucheza mechi ya watani wa jadi Simba Vs Yanga,mechi ambayo ki ukweli ni ya kumaliza ratiba na isiyo na umuhimu wowote.aliondoka David Bekham Manchester United,aliondika Thierry Henry arsenal,aliondoka Zamoyoni mogella simba akaenda Yanga na maisha ya timu yakaendelea sasa hawa viongozi wa timu zetu hawalioni hili??? mbona wengi waliondoka na timu iliendelea kwa hili mi naona viongozi wa klabu zetu waache ubinafsi na kutafuta umaarufu na kuwaachia mawakala wa wachezaji walioidhinishwa na Fifa na Tff wafanye kazi zao na kuzisaidia klabu kufanya biashara ya wachezaji ili kuweza kupata fedha za kujiendesha ili kuweze kupunguza utegemezi.klabu zetu zenyewe hazina hata mitandao?hata taarifa za klabu hazipatikani kirahisi kwa klabu kuweza kuweka rekodi za wachezaji wao na taarifa zao  sasa kwa wakala huyu anayepambana na kuiuza klabu nje ya nchi na kuweza kupata nafasi lakini viongozi hawa bado wanawawekea vizuizi ambavyo havina maana.Tuwaache wachezaji hawa  ambao ki ukweli kwa kupata timu nje ya nchi wataweza kuisaidia timu yetu ya Taifa kufikia kiwango cha juu kisoka.



Kwa hili viongozi wetu wanapaswa kujipanga na kuzisaidia klabu hizi kufikia malengo yao ya kuanzishwa na kuacha kuongoza kwa mazoea na kuishia kupiga porojo magazetini kipindi cha mechi za watani wa jadi.ni jukumu la wanachama wa klabu hizi kusema imetosha kwa viongozi wote wasiojua kuongoza soka na kuwakabidhi watu wanaoweza  kuleta maendeleo yanayoonekana ili timu hizi ziweze kujitegemea na hapo tutaweza kujenga soka bora. Bila Viongozi makini ki ukweli hatutaweza kujenga timu nzuri ya Taifa.

Kwa wakati huu ni haya tu tuonane tena wakati mwingine.

Pamoja daima .

Edwin Mac Temba Jr   +255 715 000 890
Email: mactemba@hotmail.com

No comments: