Wednesday, May 05, 2010

Kuchapa Lapa kwa Extra Bongo Kwafika Tamati


Bendi kubwa ya muziki wa dansi, Extra Bongo 'Next Level', inazidi kukwea matawi kwa kujipatia kajiusafiri ambako katafanikisha mizunguko ya kikazi ya bendi hiyo kuwa rahisi zaidi. Hii ni hatua muhimu kwa bendi hii katika kuhakikisha inamudu vyema ushindani kwa kuweka akili yao yote kwenye kuboresha kazi yao ya burudani ya muziki wa dansi. Kausafiri hako ni basi maalum.
Douglas Sagawala, ofisa habari wa bendi hiyo, amewaambia waandishi wa habari kwamba mipango ya kukabidhi basi hilo iko kwenye mstari na kazi iliyopo sasa ni kulikomboa toka bandarini kwani limeshawasili nchini.

Atakayekabidhi kifaa hicho si mwingine bali mwenyekiti na mfadhili mkubwa wa Extra Bongo, Chifu Kiumbe, ambaye ameona mbali na kuona kwamba iwapo atasitisha shughuli ya wanamuziki wake kuchapa lapa na kuwapatia kausafiri basi wataweza kuupeleka muziki wao katika levo tofauti, kwani wataweza kuweka mawazo yao yote kwenye utengenezaji wa kazi bora za muziki kwa ajili ya mashabiki wao.
Extra Bongo ambayo kwa sasa inatamba na kibao chake cha "Maisha Taiti" inatarajia kuanza ziara zake za muziki katika mkoa wa Kagera ambako siku ya Pasaka watafunga kazi katika ukumbi wa CCM, Lina Hall Bukoba mjini na Jumatatu ya Pasaka watakuwa wilaya ya Karagwe kwa ajili ya kufurahisha mashabiki wao wa huko.

No comments: