Wednesday, May 05, 2010

SOMA MAKALA HII KUHUSU MBAYUWAYU...


NAKUOMBA USOME HII MAKALA UTAJUA KINAGAUBAGA JUU YA HADITHI HII YA WAKWERE


Nilisimuliwa kisa cha mbayuwayu ambaye alikuwa anaishi katika shamba
la Mkulima mmoja huko Ukwereni. Mbayuwayu huyo aliishi na wenzake
katika maisha ya kutegemea nafaka na mbegu mbalimbali zinazopatikana
katika shamba la mkulima huyo. Pamoja naye walikuwepo ndege wengine
wengi ambao nao walipata afueni ya maisha yao katika shamba hilo zuri
la Mkwere. Miongoni mwa ndege hao walikuwepo tetere ambao walionekana
kama ndio ndege wapendwa wa mwenye shamba.

Mkulima huyo alikuwa anahakikisha kuwa tetere wanakula na kunenepa
pamoja na ndege wengine kama vile kwale na kukumaji. Na walikuwepo pia
dudumizi, vigong'ota, zokoyogo na kurumbiza. Ndege wengine wote hawa
walifurahia maisha yao katika shamba la Mkwere isipokuwa mbayuwayu.

Mbayuwayu alikuwa analalamika mara kwa mara kuwa maslahi yake
hayaangaliwi na kulindwa kama ya kina tetere. Mara kwa mara mbayuwayu
amejikuta akijitafutia riziki yake hata nje ya shamba, amekuwa
akikwepa mitego yeye mwenyewe na hata anapowindwa na paka ilimbidi
atafute mbenu endelevu za kujilinda. Katika maisha hayo mbayuwayu
alijikuta anaishi maisha ya "kiujanja ujanja" ilimradi mdomo uende
kinywani.

Mbayuwayu walikuwa wanalalamika kuwa tetere walikuwa wameachwa kula
kwa uhuru wote na wamefikia kula hata vile vidogo vya mbayuwayu.
Walilalamika kuwa hata wakionda kuna punje zimedongoka ilikuwa ni
vigumu kwani tetere walifika mara moja na kwa kutumia mabavu waliweza
hata kuwatimua mbayuwayu hao kwa kuwatishia kuwadonyoa.

Kwa vile waliona kuwa maslahi yao na maisha yao yanatishiwa na tetere
na mwenye shamba inaonekana hajali basi mbayuwayu kwa kutumia umoja
wao wa Mbayuwayu (UMBA), waliamua kuitisha mgomo wakidai maslahi zaidi
na nafasi zaidi za kutambuliwa na mwenye shamba na kupewa maslahi
ambayo yanakaribiana na yale ya tetere. Tetere waliachwa kunawiri, na
hata kujengewa matundu ya kisasa ili wao na makinda yao waishi maisha
ya raha na amani wakati mbayuwayu wakiachwa kujijengea viota vyao
kwenye kona za nyumba na majengo mbalimbali humo shambani. Tetere
walikuwa wanaruhusiwa kukaa pamoja na kuimba kwa pamoja huku wakitamba
kwa mwenye shamba kuwa;

Kuku mfupa mtupu
Mimi nyama tupu!

Hivyo mbayuwayu wakaamua kutangaza mgomo ili kumshinikiza mwenye
shamba kuangalia maslahi yao. Zikiwa zimebakia siku chache za mgomo
kufika mbayuwayu walijikuta wameweza kuwashawishi mbayuwayu wa jamii
tofauti kuweza kushiriki mgomo huo na kwa pamoja wakaanza kutangaza
juu ya ujio wa mgomo wa mbayuwayu wote shambani. Na hata siku ya
sherehe ya ndege wote wafanyao kazi zilipofika mbayuwayu waliandamana
wakiwa na mabango yaliyosomeka:

Mwenye shamba tukumbuke
Mbayuwayu na sisi tuna haki
Kwanini tetere peke yao?

Walipita siku hiyo kwa umoja mkubwa japo mwenye shamba na yeye aliamua
kufanya sherehe ya ndege wengine ambapo tetere, dudumizi, kurumbiza na
wenzake walihudhuria kwa furaha wakiburudishwa na miziki mbalimbali.
Katika sherehe ya mbayuwayu msimamo uliendelea kutolewa kuwa ni lazima
wagome kwani japo wao ni vindege vidogo na ambavyo vinaonekana havina
maana ukilinganisha na Mbayuwayu lakini vina sehemu katika maisha ya
shamba, kwani ndio vinatafuna vijidudu vidogovidogo vya hatari,
huchangamsha ndege wengine na husaidia sana katika kuhakikisha usalama
wa shamba kwani vina uwezo wa kwenda sehemu mbalimbali hata
zilizondogo na vina mwendo kasi sana kuweza kuwakwepa adui.

Hata hivyo, mwenye shamba alikasirika alipoona kuwa mbayuwayu kweli
wamedhamiria kuitisha mgomo. Yakiwa yamebakia masaa machache kabla ya
mgomo huo mkubwa kuanza mwenye shamba akaitisha mkutano wa ndege wazee
na kuanza kuwahutubia kwa ukali akielezea ni kwanini mbayuwayu
hawastahili maisha ya tetere!

Akizungumza kwa ukali na akifoka hadi mapovu yakimtoka mdomoni mwenye
shamba aliwaambia mbayuwayu kuwa yeyote atakayegoma atakiona cha moto
kwani wawindaji wote wameruhusiwa kutumia bunduki, manati na hata
mizingi ili kuhakikisha kuwa mbayuwayu hawaleti madhara katika shamba
kwa kugoma kwao. Aliwahakikishia kuwa shamba lake haliwezi kuwapa
maslahi kama ya tetere! Aliwahakikishia kuwa serikali yake ya shamba
lake haina uwezo wa kutoa maslahi kwa mbayuwayu kwani uwezo uliopo
hadi hivi sasa ni kuweza kuhakikisha tetere, dudumizi na kwale
wanaendelea kuishi maisha ambayo wanastahili.

Aliwaambia wazi kuwa hata wakigoma hatokuwa na uwezo wa kuwapa maisha
ya kitetere kwani wao ni mbayuwayu! Na akawaambia kuwa endapo watagoma
basi paka wote wa shamba watapewa leseni ya "kuwaleta wakibisha
walipuliwe". Huku akishangiliwa na ndege wazee ambao wengine hata
manyoya walikuwa hawana tena na macho yao yakisinzia kwa uchovu,
mwenye shamba aliapa kuwa kama anahitaji kura basi hizo za mbayuwayu
siyo za lazima kwani tetere na wengine wako tayari kumpatia kura zao!

Ndege wote shambani walishangaza na ukali wa mwenye shamba.
Walishangaa kwanini hajawahi kuwa mkali hivyo kwa dudumizi na mwewe
ambao wamekuwa wakila hadi vifaranga vya mbayuwayu? Walishangaa
ilikuwaje mwenye shamba awe mkali kwa mbayuwayu ambao walitaka tu
wakumbukwe kama tetere na wapewe maisha yanayokaribiana na kitetere
wakati ndege wakubwa na wenye nguvu wakiwa wanatambaa shambani na kula
mbegu na matunda yote mtini huku wakiwafukizia mbali mbayuwayu?

UMBA ilishangazwa na ukali wa mwenye shamba kwa mbayuwayu; ukali ambao
hawajawahi kuuonesha dhidi ya ndege waharibifu wa mazao ambao kwa muda
mrefu wamekuwa wakienda na kuchimbua hata mbegu zilizopandwa na kula
na kugawana? Ilikuwaje mwenye shamba awe mkali hivyo kwa mbayuwayu?

Hata hivyo, baada ya tafakari mbayuwayu wakaamua kusitisha mgomo wao;
walijua kuwa kwa kadiri ya kwamba ndege wamegawanyika kwenye shamba la
mkulima, ndege hawawezi kupata haki zao. Mbayuwayu walijua kuwa kwa
kadiri ya kwamba bado hawajaweza kuungana na kuonesha umoja wa kudai
maisha kama ya tetere na kurumbiza basi hawawezi kufurahia maisha ya
shamba hilo. Kutokana na uelewa huo mbayuwayu walidhamiria kuona kuwa
shamba hilo linaenda kwa mtu mwingine au apewe mkulima mwingine mwenye
kujali maslahi ya ndege wote siyo wale tu wenye sauti nzuri na rangi
za kuvutia kama tetere!

Mbayuwayu waliamua kurudisha majeshi yao nyuma huku wakiruka ruka
kivyao wakiimbiana na kupeana pole kwa sauti za chini ambazo mwenye
shamba hakuweza kuzisikia;

Pole mbayuwayu
Maskini mbayuwayu
Laiti ungelikuwa tetere!
Labda angekujali Mkwere!

SHUKRANI KWA M.M. MWANAKIJIJI

No comments: