Friday, May 07, 2010

Chokoraa ameziba pengo la Choki, Banza


RAPA nyota wa kundi la African Stars ‘Twanga Pepeta’, Khalid Chuma anayefahamika zaidi kwa jina la kisanii kama Chokoraa (pichani, kushoto), amefanikiwa kuwafanya mashabiki wa bendi hiyo kuwasahau wakali wa zamani walioondoka, kama vile Ally Choki na Ramadhan Masanja ‘Banzastone’.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa kwa kuwashirikisha mashabiki kadhaa wa bendi hiyo ambayo kwa sasa imerejea kileleni, ikiiengua FM Academia iliyokaa kwa kipindi kirefu, rapa huyo ndiye anayeongoza kwa kupendwa na wapenzi wa kundi hilo ambalo kwa sasa linatamba na mtindo wake wa Sugua Kisigino.

“Siyo siri, kwa sasa huyu jamaa ndiyo roho ya Twanga. Ni kweli kwamba kuna waimbaji na marapa wengi wazuri katika bendi, lakini mnyonge mnyongeni ila haki yake mpeni, Chokoraa kwa sasa yupo juu,” alisema mmoja wa mashabiki wa kundi hilo, katika onyesho la juzi Jumamosi, Mango Garden.

Hali ya rapa huyo, ambaye pia ni mtunzi na mwimbaji kuonekana muhimu kwa bendi hiyo, inatokana na hali ya sasa ambapo kila kundi hilo linapofanya onyesho lake, mwanamuziki huyo ameonekana kuwakuna zaidi mashabiki kuliko wengine.

No comments: