Thursday, October 22, 2009

MPINZANI WA FALLY IPUPA KUJA BONGO NOVEMBA




MWANAMUZIKI mahiri wa Kongo, Ferre Gola Bataringe anatarajiwa kuwasili nchini mwezi ujao kwa onyesho moja la muziki litakalofanyika mjini Dar es Salaam.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano, Udhamini na Matukio wa kampuni ya New Habari (2006) Limited, Petter Mwendapole alisema mjini Dar es Salaam jana kwamba mwanamuziki huyo atambatana na kundi la wanamuziki 17.

“Ferre atakuwepo hapa mwezi ujao kwa onyesho moja la muziki baada ya hapo atakwenda Burundi na Rwanda kwa ajili ya onyesho moja moja katika nchi hizo,” alisema.

Mwendapole alisema maonyesho ya Rwanda na Burundi yatakuwa maalum kwa ajili ya kuzindua uuzaji wa tiketi za bahati nasibu ya shindano la Miss East Africa.

Katika msafara huo pia watakuwepo wanenguaji wa kike watano ambao ni Sabena wa Kayembe, Vick Moleka, Nancy Mbemba, Renate Kunga na Patricia Isako.

‘Kuhusu tarehe ya onyesho na wapi onyesho litafanyika, tutatangaza siku ambayo tunatangaza mdhamini mkuu wa onyesho hili ambalo ni la kwanza Ferre kufanya peke yake Tanzania…hii pia ni ziara ya kwanza kwa Ferre kwa Afrika Mashariki tangu ajitoe Quarter Latin Internationale ya Koffi Olomide,” alisema.

Kabla ya kuanzisha bendi yake, Ferre aliwahi kupigia bendi ya Wenge Musica BCGB ambapo alikuja nayo nchini mwaka 1997, baadaye akabaki na kundi liliunda Wenge Maison Merre ya Werrason iliyomeguka kutoka BCBG akatembelea tena mwaka 2000.

Kisha akajiondoa na kuanzisha Le Marquizer de Maison Merre akiwa na repa Bill Caludji Clinton na Baby Ndombe, kabla ya kuchukuliwa na Koffi Olomide. Kwa sasa anatamba na albamu zake Sens Interdit, Lubukulumu na Queist Derrierur Toi yaani nani yuko nyuma yako ambayo ni albamu yake mpya.

No comments: