Monday, November 26, 2007

BASATA, kwa Wasanii tatizo ni wadosi tu…

Edwin Mac Temba Jr

Siku moja katika mkutano wa kutangaza zoezi la utoaji wa tuzo za Kili Tanzania, Afisa mmoja wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA),Ndugu Ngelo Luhala pamoja na mambo mengine alizungumzia tatizo sugu la wizi wa kazi za wasanii.

Afisa huyo alisema kwamba, kinachosababisha wasanii nchini waibiwe kazi zao ni kutoielewa mikataba wanayosaini kutokana na elimu duni waliyo nayo wengi wao.

Alitoa mfano wa msanii moja aliyeingia mkataba na kampuni moja ambao umetayarishwa kwa lugha ya Kiingereza ambayo msanii huyo haijui.

Anasema mkataba ulikuwa unaeleza kwamba, ikitokea aina yoyote ya msuguano, msanii huyo itambidi akafungue mashitaka Uingereza.

Kwa sababu hiyo, Afisa wa BASATA alidai uduni wa elimu na kutoitambua vizuri mikataba wanayosaini, ni tatizo linalochangia kwa kiasi kikubwa kuendelea kuibiwa kwa haki zao.

Inawezekana sababu hiyo iliyoolezwa na afisa huyo wa BASATA ikawa moja ya sababu, lakini ukweli ni kwamba, kilio hasa cha wasanii si juu ya mikataba, wala lugha.

Kilio ambacho wasanii wamekuwa wakikizungumzia kila siku ni mawakala wa kazi zao hususani kampuni mbili maarufu zinazomilikiwa na Watanzania wenye asili ya Kiasia, maarufu kwa jina la wadosi.

Wasanii wanadai kwamba wadosi wanawanyonya, imefikia hatua vijana wanaamua kuacha muziki kwa sababu ya hao wanaowaita wadosi.

Toleo la Machi 6,2006 la gazeti hili la Sayari katika ukurasa wake wa tatu, kulikuwa kuna habari kuhusu msanii maarufu wa muziki wa Hip hop, Juma Mohamed Mchopanga ‘Jay Moe’ aliyedai kwamba ameamua kuacha muziki.

Kisa? Amechoka kuwanufaisha wadosi, anaona anafanya kazi bure kwa kuumiza kichwa chake akichukua muda mwingi kufikiria, kutunga na kurekodi, lakini kwenye mauzo hapati chochote cha maana.

Hiyo ndiyo sababu tosha iliyomfanya aamue kuachana na muziki, lakini si Jay Moe peke yake, gwiji Mr. II naye aliwahi kutangaza kuacha muziki miaka miwili mitatu iliyopita kabla ya kurejea, sababu ikiwa ni hiyo hiyo.

Mr. II aliwahi kuzungumza huku analengwa na machozi juu ya wadosi, alielezea kwa masikitiko jinsi alivyoacha albamu yake iitwayo Itikadi wakati anakwenda Uingereza mwaka 2002, lakini aliporejea 2004, alipowafuata wadosi hao, walidai kuwa hawakuuza chochote zaidi ya nakala 5000 za mwanzo ambazo pesa yake alikwishalipwa.

Hata kwa mshabiki wa kawaida wa muziki, anaweza ‘ku-doubt’ eti albamu nzuri zinazohusisha magwiji wengine kama Dk. Remmy, King Kiki, Stara Thomas na wengineo ziuze nakala 5000 tu!

Achana na hao, msanii nyota nchini Khaleed Mohamed ‘TID’, naye aliwahi kutoka kwenye ofisi za Wadosi akiwa anazungumza peke yake mithili ya mwehu, kisa kuambiwa kuwa kazi yake ilikuwa na mauzo finyu.

TID alisikitika kuambiwa kwamba, albamu yake iitwayo Burudani yenye vibao motomoto kama vile Watasema Sana, Nakupenda na kadhalika, imeuza nakala 5000 tu baada ya miezi kadhaa kupita wakati kanda za albamu hiyo zilikuwa zimetapakaa nchi nzima.

Kila msanii nchini kilio chake ni juu ya wadosi, hivyo BASATA inaposema kwamba tatizo la wasanii ni elimu na kutoijua mikataba, ni kitu kisichoingia akilini.

Inawezekana ni moja wapo, lakini hebu tuangalie, aina ya wasanii kama TID, Mr. II, Jay Moe kweli wanaweza kusaini mikataba wasiyoielewa?

Mr. II ingawa elimu yake ni kidato cha Nne, lakini uzoefu wake wa kutembea nchi kadhaa pamoja na kujiendeleza kielimu kwa njia mbalimbali, umemfanya ajue zaidi kuhusu biashara ya muziki kwa ujumla.

Jay Moe na TID wote wamemaliza kidato cha Sita, Je, ni kweli hawa watakuwa hawajui Kiingereza kiasi cha kuingizwa mkenge kama alivyoelezea Luhala?

Hapana shaka muda umefika kwa BASATA kuwasaidia wanamuziki kwa kuanza kung’amua kilio halisi kinachowakabili wanamuziki pamoja na matatizo mengine ya uvutaji bangi, elimu dunia na kadhalika.

Sanaa ni ajira, msanii anapoamua kutumia kipaji chake kama ajira anakuwa anaipunguzia mzigo mkubwa serikali yake.

Kwa sababu mbali ya kumpatia msanii mwenyewe ajira, kuna watu wengine zaidi ya sita ambao kwa namma moja au nyngine anawapa ajira inayotokana na kipaji chake.

Bila ya msanii eti ni mtu gani atakayeweza kufungua studio ya kurekodi muziki? Kama yupo itatumika kwa kazi gani?

Bila ya msanii mtayarishaji (producer) wa nyimbo atakuwa na kazi gani?

Wafanyakazi wote wa studio kuanzia mlinzi wa getini, wote hawa ajira yao inaanzia kwa msanii.

Na hao hao mawakala wanaolalamikiwa, bila ya muziki wangefanya biashara hiyo kwa lengo gani?

Wamachinga nao wanaouza kanda kwenye matololi, bila ya msanii wangeuza samaki?

Ma-Dj wa klabu na redioni, wote hawa kazi yao ni kupiga muziki, sasa bila ya msanii watakuwa wana kazi gani hawa nao?

Kampuni za ku-shoot video za nyimbo, zimekuja kwa wingi hivi sasa nchini, chanzo chake mwanamuziki.

Hata magazeti mengi nchini hivi sasa yanategemea kuandika habari za wasanii ili yauze kwa wingi.

Kwa mantiki hiyo, sanaa inatoa wigo mpana wa ajira, hivyo inahitaji kulindwa ili iendelee kuwa nguzo muhimu kwa jamii.

Ukiacha faida zote hizo kuhusu sanaa ya muziki, zipo nyingine nyingi kama kuwaunganisha watu pamoja, kuburudisha, kuliwaza na kadhalika.

Kwa sababu hiyo, ndiyo maana leo kuna tuzo za muziki kila pembe ya dunia, ni kutokana na umuhimu wao mkubwa kwa jamii ndiyo sababu wanatuzwa.

Kwa sababu hiyo, BASATA isiwe inachukulia juu juu matatizo ya wasanii nchini, ijizamishe ndani zaidi na kufanya tathmini ya kina iyakayoiwezesha kupata jibu sahihi ambalo litakuwa tiba tosha ya ugonjwa uliopo.

Wanamuziki wanapendelea biashara ya kusambaza kanda za muziki ipanuliwe, na wapatikana mawakala wengine kama wanne au watano, ambao wataleta ushindani kwenye biashara hiyo.

Ushindani utasaidia kuwafanya hao wanaoitwa wadosi, waamke kwani mbali ya kilio cha wasanii kunyonywa na wadosi pia wanalalamika manyanyaso.

Wananyanyaswaje? Wanasema kwamba wanapokamilisha albamu zao wakizipeleka kwa wadosi, wanaambiwa wapange foleni, wasubiri, wapo ambao wamekuwa wakisubiri tangu 2002.

Hata hao wanaosema wanauza nakala 5000 na huku wakilalamika wana unafuu mkubwa kwani wapo ndugu zangu kina Super Phaby, ambao hata nakala 1000 hazifiki.

Sasa ukitathmini kwa makini, gharama pekee za studio kwa albamu nzima si chini ya Sh. Milioni moja, ambayo ni sawa na mauzo ya nakala 5000, je, huyu anayeuza nakala 1000, studio kapewa bure?

Wakati huyu anayeuza 5000, hapati faida, je mwenye kuuza chini ya nakala atapata faida gani?

Kitu pekee ambacho Chama cha haki Miliki Tanzania (COSOTA) kinaweza kusaidia ni kuwabana wezi wa mitaani, si aina wizi unaolalamikiwa na wasanii.

Wanacholalamika wasanii ni wizi wa kimachomacho, wizi usio na ushahidi ambao huwezi kwenda kumbana mtu popote pale, kwa sababu msanii japo anajua ananyonywa, lakini anabanwa na suala la sehemu gani nyingine akauze kazi yake? Hana jinsi zaidi ya kukubali achapiwe nakala 5000.

Ukibahatika kurudia kugonga muhuri, basi wewe kijukuu cha mtume, kwa sababu hiyo ndiyo maana muziki unawashinda vijana.

Kuanzishwa kwa signal maalum ya kugonga kwenye kanda, nadhani siyo dawa tosha, Serikali iangalie uwezekano wa kupatikana mitambo maalumu wa kutengenezea kanda, ili kupunguza urasimu unaolalamikiwa dhidi ya wadosi.

Hivyo kilio cha wasanii ambacho BASATA inapaswa kukifahamu na kukitafutia ufumbuzi ni si kingine zaidi ya hawa wadosi.

Pamoja we can make changes,so its time for that now!!!

No comments: